Mamlaka ya Udhibiti Ubora Tanzania (TBS) imezungumza kuhusu taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii juu ya kiwanda cha Mr and Mrs Jonsson-Johnsson Varmland Hagfors kuzalisha unga wa mahindi (sembe) ujulikanao kwa jina la Jonsson Lishe- Sembe Mswed unaosemekana kuwekwa madawa ya kuua nguvu za kiume na kuongezea hormones za ushoga.
TBS imesema mzalishaji huyo anamiliki kiwanda cha kuzalisha unga wa mahindi ulioongezewa virutubisho (fortified maize flour) kilichopo Lushoto mkoani Tanga, ambacho ubora wa bidhaa zake vimethibitishwa na TBS na kupewa Leseni ya kutumia alama ya Ubora yenye namba 5657, hata hivyo kiwanda hicho kilisimamisha uzalishaji tangu mwezi Januari 2024 kutokana na kukosa malighafi.
Baada ya uchunguzi TBS imebaini kuwa mzalishaji huyo amefungua kiwanda kingine nyumbani kwake, Bagamoyo mkoani Pwani, kinachozalisha unga wa mahindi ulioongezewa virutubisho (fortified maize flour), ambacho kilifanyiwa ukaguzi na kugundulika kuwa hakijathibitishwa na TBS.
Hata hivyo TBS imesema ilichukua sampuli ya unga wa mahindi unaozalishwa na kiwanda cha Bagamoyo na kuifanyia uchunguzi wa kimaabara na kuthibitisha kuwa imeongezewa virutubisho kwa mujibu wa kiwango cha bidhaa hiyo, ambapo imeeleza kuwa utaratibu wa kuongeza virutubisho vya vitamini na madini kwenye unga wa mahindi, unakubalika kwa mujibu wa Kiwango cha Kitaifa na hufanyika kwa lengo la kuboresha hali ya lishe kwa walaji.