Watu nane (Wanaume saba na Mwanamke mmoja) Wakazi wa Kijiji cha Kambai kilichopo Kata ya Kwezitu Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga wamefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Muheza muda huu leo April 05,2024 wakishtakiwa kwa kosa la kuchoma gari la Afisa Kilimo wa Kata ya Tongwe aina ya Suzuki pamoja na kumjeruhi Afisa huyo wakimtuhumu kushindwa kusimamia maslahi ya Wananchi na kupelekea Wawekezaji kupewa eneo la zaidi ya ekari 500 bila tathmini ya kina kufanyika wala Wananchi kushirikishwa.
Itakumbukwa jana @AyoTV_ iliripoti tukio hilo ambapo baadaye Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah baada tu ya kupokea taarifa hizo alilazimika kufika katika Kijiji hicho ili kufanya mkutano na Wananchi kwa lengo la kutafutia ufumbuzi suala hilo huku akithibitisha kuwa Afisa kilimo amejeruhiwa na amelazwa Hospitali ya Wilaya Muheza akipatiwa matibabu.
“Halmashauri ina eneo zaidi ya ekari elfu 3 lenye hati kwa zaidi ya miaka 28 lakini ndani ya kipindi cha miaka hiyo zaidi ya 28 hawajaliendeleza, alipatikana Mwekezaji wa kwanza mwaka 2020/2021 akapewa ekari 500 pasipo tathmini ya kina kufanyika kujua kiwango cha uvamizi kilichofanyika kwenye eneo hilo, mwaka jana 2023 wamepatikana Wawekezaji wengine wanne nao pia tathmini ya kina haikufanyika”