Afisa wa Hamas aliliambia shirika la habari la Reuters siku ya Jumatatu kuwa hakuna maendeleo yoyote yaliyofikiwa katika duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza mjini Cairo ambayo pia yamehudhuriwa na wajumbe kutoka Israel, Qatar na Marekani.
“Hakuna mabadiliko katika nafasi ya uvamizi na kwa hivyo, hakuna jipya katika mazungumzo ya Cairo,” afisa wa Hamas, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia Reuters.
“Bado hakuna maendeleo,” aliongeza.
Mapema Jumatatu, kanali ya televisheni ya taifa ya Misri ya Al-Qahera News TV ilinukuu chanzo kikuu cha Misri kikisema maendeleo yamepatikana katika mazungumzo hayo, baada ya kufikiwa makubaliano kati ya wajumbe walioshiriki katika masuala yanayojadiliwa.
Israel na Hamas walituma timu nchini Misri siku ya Jumapili baada ya kuwasili siku ya Jumamosi Mkurugenzi wa CIA William Burns, ambaye uwepo wake ulisisitiza shinikizo la Marekani kwa ajili ya makubaliano ambayo yatawaachilia mateka walioko Gaza na kupunguza mzozo wa kibinadamu huko.