Mbunge wa Viti maalum Mhe Khadija Shabani Taya amempa tano Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhimiza Nishati safi ya kupikia ikiwa ni agenda ya kumtua Mama kuni kichwani.
Hiyo ni miongoni mwa mkakati jumuishi wa kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili mpaka kufikia 2033 wananchi zaidi ya 80% wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi na mkaa ulioboreshwa.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi 200 kwa watu wenye ulemavu mkoa wa Dodoma iliyofanyika jana tarehe 7 Aprili 2024, Mbunge Keysha amesema kilichofanyika ni mwendelezo wa kile ambacho amekuwa akikifanya kwa watu wenye Ulemavu ikiwemo kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi Changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Mbunge Keysha amemshukuru Rais Samia kwa kuwajali watanzania hususani watu wenye ulemavu nchini.
“Na Mimi ninapoendelea kusema pale Bungeni haina maana kwamba sifurahishwi na mambo ambayo yamefanywa lakini jinsi ambavyo changamoto zinapozidi kutatuliwa ndivyo ambavyo changamoto zingine zinaendelea kuonekana, hatuna nia mbaya, nia yetu ni kujenga” amekaririwa Mhe Khadija
Katika hafla hiyo iliyoambatana na chakula cha jioni ikiwa ni sehemu ya iftar iliyofanyika katika viwanja vya CCM Mkoa wa Dodoma Mbunge Khadija ameiomba Serikali kurejesha asilimia mbili ambayo anaamini kuwa ni ukombozi kwa watu wenye ulemavu katika kujikwamua kimaisha na kiuchumi.