Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa taarifa kuhusu tukio la kuzama kwa meli iitwayo MV Maman Benita iliyotokea katika Ziwa Tanganyika ambapo limesema meli hiyo iliyosajiliwa chini ya bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, inamilikiwa na kampuni ya Kikongo, iitwayo Etablissement Manimani.
“Meli hiyo iliyoanza safari yake tarehe 6 Aprili 2024 majira ya saa 12:00 jioni ikitokea bandari ya Kigoma kuelekea Kalemie, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikuwa imebeba jumla ya abiria 27 wakiwemo Watanzania watano, Wachina wanne , Raia wa Kongo 16, Raia mmoja wa Kenya pamoja na Mtoto mdogo”
“Meli hiyo iliyotarajiwa kuwasili Kalemie majira ya saa 8:00 usiku, haikufika ambapo asubuhi ya tarehe 7 Aprili 2024, wavuvi walifanikiwa kumwokoa abiria mmoja mwenye asili ya China na kisha kutoa tarifa kwa Mamlaka za Serikali ya Kongo juu ya kuzama kwa meli ya MV Maman Benita katika eneo la Kabimba, Nchini Kongo, baada ya kupata taarifa hiyo, zoezi la utafutaji na uokoaji lilianza mara moja ambapo hadi kufikia majira ya saa 1:00 usiku wa tarehe 7 April, 2024, Wahanga 17 walikuwa wameshaokolewa, kati yao ikijumuisha Wachina 2, Watanzania 3, na Wakongo 12”