Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kupitia tiba inayojulikana kama Dk. Samia Suluhu Hassan Outreach Services, imefika mikoa 13 na kutoa huduma ya moyo kwa wananchi 11,254.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano JKCI, Anna Nkinda, amesema hayo wakati akizungumzia tuzo mbili za heshima za uhusiano na mawasiliano katika kutoa elimu kwa umma kuhusu magonjwa ya moyo na kutoa huduma kwa jamii ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo ambazo JKCI ilipata.
Tuzo hizo zilitolewa jijini Dar es Salaam na Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST), mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi.
Nkinda amesema kwenye taarifa yake kuwa JKCI imeshinda tuzo hizo kupitia huduma za tiba mkoba zinazojulikana kwa jina la Dk. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inazozifanya kwa kufanya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo.
Amesema upimaji huo unakwenda pamoja na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo na matumizi sahihi ya dawa za moyo, kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa jinsi ya kuwatambua wagonjwa wa moyo na kufanya utafiti wa magonjwa ya moyo.
Amesema ushindi huo pia umetokana na mchango mkubwa unaotolewa na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano katika kuuhabarisha umma kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi pamoja na kutoa elimu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi.