Chama cha ACT Wazalendo kimemtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, afike Rufiji na Kibiti, mkoani Pwani kuona hali halisi na kuhakikisha hatua stahiki na haraka zinachukuliwa kunusuru wananchi waliokumbwa na mafuriko.
Kimesema mafuriko hayo yametokana na kuzidiwa kwa Bwawa la Mradi wa Kufua Umeme kwa Maji la Julius Nyerere (JNHPP), hivyo kulazimika kuifungua milango minne ili kuyapunguza, jambo lililosababisha maji kufurika katika makazi na baadhi ya mashamba ya watu.
Mkoani Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita ametoa kauli hiyo akitaka serikali kuweka mpango wa kukabiliana na maafa.
Mchinjita amesema matukio ya maafa na majanga kwa miaka ya hivi karibu yamedhihirisha uwezo mdogo wa serikali kuyakabili kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere tangu miaka ya nyuma ulitolewa tahadhari na mojawapo ilikuwa ni kudhibiti maji yasisababishe mafuriko makubwa na kuathiri wakazi jirani.
“Sasa Bwawa la Rufiji limejaa, ukisoma andiko la mradi linaeleza kutakuwa na mabwawa mengine ya kuhifadhia maji yakijaa.
“Serikali kwa kujiambia yenyewe bila kufuata taarifa za Mamlaka ya Hali Hewa (TMA) na wataalamu ikadhani itajaza bwawa hilo kwa miaka mitatu.
“Kwahiyo, wakaanza kujaza bila kuwa na hayo mabwawa ya akiba, matokeo yake mwaka huu kumekuwa na mvua kubwa, maji yamejaa kwa kiwango ambacho wakiacha bila kuyatoa litapasuka na litafunika Rufiji yote,” amesema Mchinjita.
“Mashamba ya wakulima yote yamegeuka ziwa, sasa serikali imeanza kujitetea kwamba haihusiki, ninataka kusisitiza serikali inapaswa kuwajibika katika hili.
“Ukanda wa Kibiti na Rufiji eneo linalozunguka Bonde la Mto Rufiji, hasa lililoko karibu na bwawa la kuzalisha umeme kuna hali mbaya sana, zaidi ya kata 12 zimeathirika vibaya na maji, mazao, makazi, huduma za msingi za kijamii zimeharibiwa, wananchi wengi wamejihifadhi kwenye shule ambazo hazijapatwa na maji, hali ni mbaya,” amesema.