Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu Mhe. Zainabu Katimba amewataka watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo ya Elimu nchini.
Mhe. Katimba ametoa kauli hiyo tarehe 08 Aprili, 2024 wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), unaofanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kiwete jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa TSC ndiyo yenye dhamana ya kusimamia walimu ambao wanachukua zaidi ya nusu ya Watumishi wa Umma nchini, hivyo ni vema kufanya kazi kwa bidii ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa amani na utulivu.
“Katika kipindi cha uongozi wake tumeshuhudia akitoa kipaumbele kikubwa katika Sekta ya Elimu, watumishi wa umma wamepandishwa vyeo kwa mfululizo,”amesema.
Amesema katika kudhihirisha hilo, walimu 227,383 wamepandishwa vyeo na walimu 37,879 waliajiriwa katika uongozi wa Rais Samia.
“Ukiangalia juhudi hizo za Rais wetu, ni muhimu kwenu ninyi watumishi kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake kikamilifu na kusaidia kutatua changamoto zinazorudisha nyuma utendaji kazi wa walimu,”ameongeza.
Aidha ameipongeza TSC kwa kujenga mfumo wa kielektoniki wa Teachers’ Service Commission Management Information System (TSCMIS), kusimika mtandao wa intaneti kwenye baadhi ya Ofisi za Wilaya pamoja na kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la TSC Makao Makuu ambalo limefikia asilimia 37.