Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe.Zainab Katimba amesema katika mwaka wa fedha 2023/24 jumla ya Shilingi milioni 435 zimetumika katika ujenzi wa madaraja katika barabara ya Mpetu-Matongo, Misugha-Msule-Sambaru, Mungaa-Ntuntu-Mang’onyi na Lighwa-Ujaire na utekelezaji wake umefikia asilimia 90.
Mhe. Katimba ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Mhe Miraji Mtaturu aliyehoji ni lini Serikali itajenga madaraja kwenye barabara za Misughaa-Kikio na Matongo-Mpetu-Singida.
“ Serikali kupitia kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA imeweka katika mpango wake kwa mwaka wa fedha 2024/25 jumla ya Sh Bilioni 1.1 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja katika Wilaya ya Ikungi.
Katika barabara za Misughaa-Kiko na Matongo-Mpetu kuna uhitaji wa jumla ya madaraja matatu ambayo ni Daraja la Mto Matongo lenye urefu wa mita 65, Daraja la mto Isanja lenye urefu wa mita 45 na Daraja la mto Siuyu lenye urefu wa mita 30.
Kutokana na ukubwa wa madaraja haya usanifu wa kina unahitajika kufanywa ma TARURA tayari imeshaanza kutekeleza kazi ya usanifu wa madaraja haya kwa lengo la kupata gharama halisi za ujenzi wake,” Amesema Mhe Katimba