Maandalizi ya kuitishwa Uchaguzi Mkuu wa mwezi Disemba mwaka huu nchini Sudan Kusini yanaendelea huku juhudi zikifanyika kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na katika maeneo mengi zaidi ya nchi hiyo.
Baada ya kusitishwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2018, vita vya kuwania madaraka ambavyo vilizuka baada ya nchi hiyo kujitenga na Sudan mwaka 2011, ratiba ya kwanza ya Uchaguzi Mkuu wa Sudan Kusini ilipangwa kuwa kabla ya mwezi Februari 2023. Hata hivyo, serikali ya mpito na kambi ya upinzani walikubaliana kuakhirisha uchaguzi huo hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2024.
Abednego Akok Kacuol, mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Sudan Kusini, amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa kitaifa wa Juba kwamba, wamesambaza maafisa wao katika pembe zote za nchi hiyo na pia wameshapata baadhi ya magari ambayo ni muhimu katika kufanikisha zoezi hilo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Sudan Kusini imepanga kufanya Uchaguzi Mkuu mwezi Disemba yaani mwishoni mwa kipindi cha serikali ya mpito kilichokuja baada ya vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka muda mfupi baada ya Sudan Kusini kujitenga na Sudan mwaka 2011.
Vita hivyo vya uchu wa madaraka baina ya Rais Salva Kiir na makamo wake Riek Machar vimegharimu maisha ya takriban watu 400,000.