Vyama vya siasa na mashirika ya kiraia nchini Mali Alhamisi yametupilia mbali kwa pamoja amri ya utawala wa kijeshi ya kusimamisha shughuli za kisiasa na yameapa kuweka pingamizi ya kisheria dhidi ya kile mwanasiasa mmoja wa upinzani amekitaja kuwa “hatua ya kidikteta.
Taifa hilo la Afrika Magharibi limekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu mapinduzi ya 2020. Mvutano umeongezeka katika wiki za hivi karibuni, na kupelekea vyama vikuu vya siasa na mashirika mengine kuukemea kwa pamoja uongozi wa kijeshi tarehe 31 Machi kwa kutoitisha uchaguzi ndani ya muda uliopangwa.
Utawala wa kijeshi Jumatano ulitoa amri ya kusimamisha shughuli za vyama vya siasa hadi itakapotolewa taarifa nyingine kwa madai ya kutaka kudumisha usalama wa umma.
Wakijiunga pamoja, vyama vya siasa na makundi ya kiraia yamesema kushangazwa na uamuzi huo na kuuita kuwa “ukiukwaji mkubwa” wa uhuru wa kidemokrasia”.
Waliosaini tangazo hilo wamesema wanatupilia mbali amri hiyo na wataipinga mahakamani na wamekataa kushiriki katika shughuli yoyote ya serikali ikiwemo mjadala wa kitaifa unaoendelea.
Wakati huo huo uongozi wa kijeshi Alhamisi umepiga marufuku vyombo vya habari kuripoti kuhusu shughuli za vyama vya siasa.