Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt. Yusuph Ngenya amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TBS kwa waandishi wa habari na wahariri hii leo 15 April 2024.
Moja ya majukumu yake ikiwa ni kusimamia viwango vya ubora vilivyotangazwa kwa kutumia mifumo mbalimbali ya udhibiti ubora kama vile ukaguzi na upimaji wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuja nchini, upimaji wa bidhaa kwa kuzingatia matakwa ya kiwango au ya mzalishaji na usajili wa mifumo ya ubora na kipaumbele kilichowekwa katika viwango vya kitaifa ikiwa katika nyanja za nguo, ngozi, kilimo na chakula, madawa (kemikali), uhandisi na mazingira;
Kwa upande mwingine TRA inatarajia kuanza ujenzi wa maabara ya kisasa katika kanda ya Ziwa (Mwanza) na kanda ya kaskazini (Arusha). Maabara ya kanda ya ziwa inatarajiwa kuhudumia mikoa sita (6) ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.
Aidha, maabara ya kanda ya Kaskazini inatarajiwa kuhudumia mikoa minne (4) ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Shirika limeandaa utaratibu wa kukagua viwanda vyote hapa nchini ili kuhakikisha kwamba vinazalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa.
Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000.
Shirika la TBS pia limetengeneza mifumo ya kielektroniki inayotumika kutoa huduma zake,uanzishwaji wa mifumo ya kielektroniki imewezesha wateja kupata huduma za TBS popote walipo kwa wepesi na haraka hivyo kupunguza gharama kwa wateja.
‘Serikali kwa kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya milioni 250 kwa dhumuni la kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote huku kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000. Kati ya leseni hizo, jumla ya leseni 1,051 zilitolewa bure na kwa Wajasiriamali wadogo’Dkt. Yusuph Ngenya