Mkurugenzi wa Huduma za Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amewaomba wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuunda timu za ukaguzi wa vifaa tiba vinavyonunuliwa katika vituo vya kutolea huduma za Afya ya msingi.
Dkt. Mfaume ametoa maelekezo hayo baada ya kukagua shughuli za uendeshaji huduma za Afya katika Hospitali ya Halmashauri ya Misenyi na kubaini kuwepo kwa vifaa vilivyonunuliwa kutoka kwa mdhabuni na kukabidhiwa bila kukaguliwa na timu ya usimamizi wa Huduma za Afya ngazi ya halmashauri (CHMT).
Aidha,Dkt. Mfaume ameshangazwa na kasi ya ununuzi wa vifaa hivyo kutoka kwa mdhabuni na kupokelewa bila kukaguliwa na baadae kutunzwa kwa muda mrefu pasipokufungwa na kuanza kutoa huduma.
“Kinachonishangaza kwanini wamekimbizana kwenye kununua na ‘speed’ imekuwa kubwa lakini vifaa vimefika hapa lakini ile ‘speed’ ya kuvipeleka kwenye matumizi haipo tena na wanakimbizana kwenye manunuzi hata hawajahangaika kuangalia kilicholetwa kina ubora hapa kuna mashine mbili za kufulia hazijakaguliwa nawamemlipa mdhabuni milioni 90” amesema” amesema Dkt. Mfaume
Katika kusisitiza hilo ametoa muda wa siku mbili kwa CHMT ya Halmashauri ya Misenyi kujitathmini kiutendaji na kuhakikisha vifaa hivyo kufungwa na kuanza kutumika.
Timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI ikiongozwa na Dkt. Mfaume ipo mkoani Kagera kwaajili ya usimamizi shirikishi na ukaguzi wa huduma katika maeneo ya kutolea huduma za Afya.