Waziri wa katiba na Sheria Balozi Pindi Chana amewataka watumishi na wananchi nchini kutumia mifumo ya Tehama kwa usahihi ili kuepuka taarifa za upotoshaji.
Balozi Chana ameyasema hayo 15 April 2024 Kibaha mkoani Pwani katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere wakati akifungua kikao cha Baraza la wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na kusisitiza kuwa matumizi ya Tehama hasa AI (Artificial Intelligence) yasipotiliwa umakini yaweza kupotosha na kupoteza mwelekeo wa mipango thabiti ya maendeleo.
Aidha amezitaka Taasisi zilizo chini ya wizara ya katiba na sheria nchini kuhakikisha wanafanya vikao vya mabaraza ya wafanyakazi ili kutumiza matakwa ya kisheria.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya kurekebisha sheria Tanzania George Mandepo ameeleza umuhimu wa kufanyika Baraza hilo la wafanyakazi ni kwa kuwa wao ndio watekelezaji wa majukumu yote ya Taasisi huku baadhi ya wajumbe wakikao hicho wakieleza Baraza hilo linasaidia kusikiliza changamoto za watumishi hao kwa kuyatatua ili kuyafikia malengo yaliowekwa.