Justin Brady, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) nchini Sudan amesema, “leo, Sudan ni mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani huku nusu ya wakazi wa Sudan yaani watu milioni 25 wanahitaji msaada wa kibinadamu.”
Afisa huyo mkuu wa OCHA nchini Sudan akiwa Port of Sudan nchini humo, kwa njia ya video amewaeleza waandishi wa habari Ijumaa kwamba: “Mapigano makali yanapoendelea janga la kibinadamu linazidi kuwa baya zaidi siku hadi siku.
Tayari, karibu watu milioni tano wako hatua moja mbali na njaa. Na uchambuzi wa hivi majuzi unaonesha kuwa njaa inatarajiwa katika sehemu za Khartoum na Darfur, hasa katika maeneo ambayo ni magumu kufikiwa.”
Brady amesema kote Sudan, watu milioni 18, zaidi ya theluthi moja ya watu wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Hiyo ni watu milioni 10 zaidi ya wakati kama huu mwaka jana. Na kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa wakati wa msimu wa mavuno wa Sudan.”
Ameongeza kwamba, “Mapigano ni makali sana kwa watoto, inakadiriwa watoto 730,000 wanaugua utapiamlo mkali,” na kubaini kuwa, “Bila ya msaada wa haraka, zaidi ya watoto 200,000 wanaweza kufa kutokana na njaa inayotishia maisha katika wiki na miezi ijayo.”