Maafisa wa Russia wa Idara ya Kukabiliana na Majanga ya Kimaumbile wameeleza kuwa idadi ya nyumba zilizozama kutokana na mafuriko nchini humo imepindukia 15,000.
Maafisa hao wa Idara hiyo katika Wizara ya Russia ya Kushughulikia Majanga ya Dharura wameeleza kuwa maeneo ya makazi 193 katika majimbo 33 ya nchi hiyo yameathiriwa na mafuriko ya mto.
Wameeleza kuwa idadi ya nyumba zilizozama sasa inafikia 15,641, na zaidi ya bustani 4,000 pia zimeathiriwa na mafuriko.
Taarifa kutoka Manispaa ya Kurgan imeeleza kuwa maji ya mafuriko yalikuwa yakielekea mjini, na hivyo kupelekea kutolewa wito wa kuhamishwa kwa wananchi katika maeneo salama haraka iwezekanavyo.
Tayari zoezi la uokoaji limeanza katika makazi manane katika mkoa wa Tyumen, ambapo hali ya hatari ilitangazwa kutokana na tishio la mafuriko.
Gavana wa Mkoa wa Tyumen, Aleksandr Moor amesema kuwa kiwango cha maji katika Mto Ishim kinaweza kufikia mita 10.
Itakumbukuwa kuwa nyumba zaidi ya 2,400 zilizama katika jiji la Orsk katika mkoa wa Orenburg huko Russia baada ya bwawa la Mto Ural kupasuka jioni ya tarehe 6 mwezi huu wa Aprili.
Rais Vladimir Putin wa Russia wiki iliyopita aliiagiza serikali kuunda kamati maalumu ya kushughulikia maafa ya mafuriko.