Rais wa Tanzania ametangaza kurejesha tena utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kuanzia July, 2024 kwa utaratibu wa kutumia Benki kwa Halmashauri 10 za majaribio ambazo ni Majiji ya Dar es Salaam na Dodoma, Manispaa za Kigoma Ujiji na Songea, Miji ya Newala na Mbulu, Wilaya za Siha, Nkasi, Itilima na Bumbuli.
Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa ametoa taarifa hiyo Bungeni Jijini Dodoma leo April 16,2024 wakati akitoa hotuba kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2024/2025 ambapo amesema Halmashauri 174 zilizobaki zitatumia utaratibu ulioboreshwa ili kuondoa mapungufu yaliyosababisha changamoto za awali ambazo zilipelekea Rais Samia kusitisha mikopo hiyo kwa muda ili iboreshwe .
Utaratibu ulioboreshwa unahusisha uanzishwaji wa kitengo cha usimamizi wa mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI, na uanzishwaji wa kamati za usimamizi wa mikopo katika ngazi za Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Halmashauri na Kata ambapo majukumu ya Kamati ngazi ya Kata ni kutambua Waombaji na kuthibitisha vikundi vya mikopo na kuvisajili kwenye mfumo kabla ya kuwasilisha kwenye Kamati ya Halmashauri.
“Kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kusanifu na kujenga mfumo mpya unaoitwa Wezesha Portal utakaotumika kwa ajili ya taratibu za ukopeshwaji wa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu, mfumo huu utaondoa changamoto za mfumo zilizokuwepo awali kabla ya mikopo kusimamishwa, maboresho mengine ni kujenga uwezo kwa Wasimamizi wa mikopo hiyo kwa kuongeza idadi ya Wasimamizi wa mikopo kwenye ngazi ya kata ambapo maafisa maendeleo ya jamii 787 wameajiriwa na kupangiwa kata zilizokuwa na upungufu.
“Mikopo inayotarajiwa kutolewa ni shilingi bilioni 227.96 ambapo shilingi bilioni 63.67 ni fedha za marejesho zilizokuwa zikiendelea kukusanywa kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamishwa, shilingi bilioni 63.24 ni fedha zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya mikopo na shilingi bilioni 101.05 ni fedha ambazo zimetengwa kutokana na makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwaka 2024/25”