Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa uwanja wa michezo wa King George Memorial uliopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro utatengenezwa ili uweze kutumika kwa ajili ya mazoezi ya timu zitakazokuwa jijini Arusha kipindi cha mashindano ya AFCON 2027.
Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma leo Aprili 16, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Mjini na Tarime Mjini waliotaka kujua mkakati wa Serikali wa kuboresha na kujenga viwanja vya Michezo ukiwemo uwanja wa Michezo Wilayani Tarime.
Mhe. Dkt. Ndumbaro ameliambia Bunge kuwa Serikali kwa sasa imejikita katika ujenzi na ukarabati wa viwanja vitakavyotumika katika mashindano ya AFCON 2027 ambavyo ni pamoja na uwanja wa Arusha, maeneo ya kupumzika Dodoma na Dar es Salaam , ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa na Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Aidha Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa Serikali inathamini Michezo yote kwa kuwa viwanja vinavyojengwa vinazingatia michezo mbalimbali ikiwemo ya kuogelea, Kikapu, riadha na netiboli na kwamba ipo tayari wakati wowote kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wamiliki na wadau mbalimbali wa michezo wanaokusudia kujenga au kuboresha miundombinu ya michezo kwa kuzingatia miongozo ya mashirikisho ya michezo husika.