Jeshi la Anga la Nigeria lilitangaza jana Jumanne kwamba mashambulizi ya anga yamewaua vinara watatu wa magaidi na magaidi wengine 30 katika Jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Msemaji wa Jeshi, Edward Gabkwet, amesema katika taarifa yake kwamba Ali Dawud, Mallam Ari na Bakurah Fallujah waliuawa pamoja na magaidi wengine waliokuwa nao mnamo Aprili 13 katika maficho ya kundi la kigaidi la ISWAP katika kijiji cha Kolleram kando ya Ziwa Chad.
Amesema magari mengi ya magaidi, pikipiki na mali ya vifaa viliharibiwa.
Halikadhalika ameeleza kuwa: “Taarifa za kijasusi zilikusanywa baada ya shambulio hilo la anga na zilionyesha zaidi kwamba shambulio hilo liliharibu kabisa kituo muhimu cha magaidi ndani ya eneo la Kolleram, ambacho kilikuwa kitovu cha shughuli za usindikaji wa chakula za magaidi, ikiwa ni pamoja na mashine za kusaga.”
Gabkwet amesisitiza kuwa shambulizo hilo lilivuruga kwa kiasi kikubwa uwezo wa kutekeleza hujuma wa kundi la kigaidi la ISWAP.
Msemaji wa Jeshi pia ameongeza kwamba: “Mashambulizi haya ya angani yanakamilisha juhudi zinazoendelea za vikosi vya nchi kavu katika Ukingo wa Ziwa Chad na kuwakilisha hatua muhimu katika mapambano dhidi ya ugaidi nchini Nigeria.”