Mnamo Desemba 03 , 2023 katika Wilaya ya Hanang yalitokea maporomoko ya tope yaliyoambatana na mawe, magogo na maji kwa wingi kutoka mlima Hanang’ kuelekea makazi ya watu maafa ambayo hayakuwa mafuriko ya maji kama ilivyozoeleka na kusababisha madhara mbalimbali ukiwemo uharibifu wa miundombinu ya maji katika kata nne ambazo ni Gendabi, Jorodom, Nangwa na Gitting,uharibifu huu ulisababisha wananchi wa kata hizo na maeneo ya jirani kukosa huduma muhimu ya maji safi na salama.
Kupitia shirika la WaterAid ikiwa ni moja ya wadau wakuu wa maswala ya maji na usafi waliitikia kwa ukubwa na kukarabati miundombinu ya chanzo cha maji iliyoathiriwa na maporomoko ya matope, mawe na magogo katika eneo la kata ya Nangwa kwa gharama ya 127,444,104 za kitanzania.
Akiongea katika hafla ya makabidhino ya mradi huu, Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid Tanzania Anna Mzinga alisema;
“Kufuatia changamoto hii iliyoikuta wilaya ya Hanang mnamo mwishoni wa mwaka 2023, ilitupelekea sisi kuwa hapa siku ya leo kwasababu ili maisha ya mwanadamu yawe na utu na stara, tunaamini anapaswa kuwa na huduma za maji safi na salama pamoja na choo bora.
‘Hivyo basi, tulisukumwa sisi kama shirika linalotekeleza miradi ya maji na usafi wa mazingira, kukarabati chanzo hiki cha maji cha Nangwa ambacho kiliharibiwa vibaya sana na mvua kubwa.” Anna Mzinga
Sambamba na ukarabati wa chanzo hiki cha maji, Shirika la WaterAid lilitoa elimu ya usafi wa mazingira na vyoo bora katika ngazi ya kaya kwa watoa huduma za afya, wenyeviti wa kata na vijiji ili jamii kuwa na utayari wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.