Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora inatarajia kuajiri watumishi wapya 46,000 katika kada ya Elimu,Afya na kada nyingine kabla ya mwezi juni baada ya Rais kutoa kibali hicho April 16, 2024.
Taarifa hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora George Simbachawene katika kipindi cha maswali na majibu kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Bernadeta Mushashu aliyetaka kujua serikali inampango gani wa kupeleka walimu katika shule za msingi na sekondari.
“Rais ametoa kibali cha kuajiri watumishi 46,000 na katika idadi hiyo kibali cha ajira ya walimu ni 12,000 na ajira ya Afya ni Zaidi ya 10,000 na Imani yangu kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI tutahakikisha upungufu wa walimu kwenye maeneo yetu tutakwenda kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa na tunafikiria kuwa na utaratibu mpya wa kuajiri kupitia kwenye mikoa yetu na katika kuzingatia maoni ya wabunge” George Simbachawene
Awali akijibu swali hilo Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Zainab Katimba amesema mwezi Mei 2023 serikali iliajiri walimu 13,130 na kabla ya mwaka wa fedha 2023/24 kumalizika serikali itaajiri watumishi wengine.