Wananchi walioathiriwa na mafuriko wilayani Rufiji wameiona thamani na umuhimu wa uwepo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA baada ya leo Aprili 16, 2024 kupokea misaada mbalimbali kutoka kwa taasisi hiyo yenye thamani ya shillingi millioni 20 ikiwemo tani 6.4 za unga wa sembe, Kilo 666 za maharage na magodoro 186.
Kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA akimkabidhi misaada hiyo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge, Kamishna Msaidizi mwandamizi Abraham Jullu amesema TAWA imeguswa na janga la mafuriko lililowapata majirani na wadau namba moja wa uhifadhi wananchi wa Rufiji ambao wamehusika kwa kiasi kikubwa kulinda rasilimali za Hifadhi ya Selous na hivyo imelazimika kuwashika mkono.
Jullu amesema tangu changamoto hii ya mafuriko imejitokeza TAWA ilifika kwa haraka na kuongeza nguvu kwa kutoa kikosi cha Askari 24 ili kusaidia katika zoezi la uokozi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya mbinu za kujikinga na madhara yatokanayo na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko kwa jamii ambapo mpaka sasa TAWA imetoa elimu hiyo kwa wananchi wapatao 4,225 na bado inaendelea na zoezi hilo.
Sanjari na hilo, TAWA imetoa boti moja lenye uwezo wa kubeba jumla ya watu 15 ili kusaidia katika shughuli za uokozi zinazoendelea wilayani humo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupeleka misaada mbalimbali kupitia Serikali na Chama Cha Mapinduzi tangu wilaya hiyo ipate changamoto hiyo ya mafuriko.