Kampuni ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, wamesaini hati ya makubaliano ya kufanya biashara ya hewa ukaa yenye lengo la kuwanufaisha wananchi wa wilaya hiyo na kutunza mazingira.
Tukio hilo la kihistoria limefanyika tarehe 17 Aprili, 2024 katika ukumbi wa hoteli ya Ruangwa Pride mjini Ruangwa na kushuhudiwa na Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, wenyekiti na watendaji wa vijiji vitakavyohusishwa na mradi huo.
Kabla ya kusainiwa kwa mkataba huo, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa walifanya kikao maalum cha kujadili makubaliano hayo na kuridhia na kuipa baraka zote halmashauri hiyo kusaini mkataba huo.
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo wa makubaliano ya kufanya biashara hiyo ya hewa ukaa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Andrew Chikongwe aliwashukuru madiwani kwa kuridhia kusainiwa kwa mkataba huo.
Chikongwe alisema tukio hilo la kusaini haki ya makubaliano lina maana ya kuwakaribisha wawezeshaji hao kuanza kufanya taratibu nyingine za kutekeleza mradi huo wenye lengo la kutunza mazingira ikiwa sambamba na kuinua kipato cha wananchi wa Ruangwa.
“Tukio la leo ni zao la safari ya mafunzo kuhusu biashara hii tuliyoifanya katika halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi, tunaishukuru sana Carbon First kwa kukubali kushirikina na sisi katika kutekeleza mradi huu wa hewa ukaa,” alisema Chikongwe.
Chikongwe alisema mradi huo ni mpya hivyo baada ya kuwakaribisha hatua ya kwanza ni kutoa elimu kwa wananchi wa vijiji 14 ambavyo vitahusika na mradi huo ili kujenga uelewa wa kutosha kabla ya kuanza kwa mradi huo.
Afisa Mkuu wa Operesheni wa Carbon First Tanzania Ltd, Iftikhar Khan ameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kuwakabirisha na amewaahidi mradi huo unaenda kubadilisha jamii nzima ya maeneo hayo.
Khan amesema baada ya kusaini hati ya makubaliano watafuata hatua nyingine kwa haraka ili wasaini mkataba kamili wa biashara hiyo kwa lengo la kutimiza adhma ya mradi huo kuinua jamii kiuchumi na kutunza mazingira.
Kwa upande wake, Mtaalam Mshauri wa Mazingira wa Carbon First Tanzania Ltd, Injinia Elisekile Mbwile alisema mbali ya kuinua uchumi wa wananachi wa Ruangwa, kikubwa mradi huo unaenda kuokoa misitu kwa kubadilisha kipato cha ukaa na mbao kugeukia hewa ukaa.
“Takwimu zinaonyesha heka 400,000 zinaharibiwa ndani ya mwaka mmoja, lakini kupitia mradi huu unaenda kuokoa misitu hiyo, kwani mwananchi badala ya kufikiria kukata mbao au mkaa, atatunza misitu ili kupata faida ya biashara ya hewa ukaa,” alisema Injinia Elisekile.
Injia Elisekile alisema mbali ya elimu wataenda kukagua aina ya miti katika misitu hiyo, umri wa miti hiyo sambamba na udongo wa maeneo husika kwa lengo la kuona uwezekano wa kupanda miti mingine.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya alisema jumla ya hekta 250,000 kutoka katika vijiji 14 zitatumiwa katika mradi huo ambao wamejipanga uanze kwa haraka iwezekano ili utoe matunda kwa wananchi wa Ruangwa.