Katika ziara hiyo, Waziri Tax alilipongeza Jeshi la Kujenga Taifa kwa jinsi linavyotekeleza majukumu yake kuchangia shughuli za maendeleo ya Taifa, malezi na mafunzo kwa Vijana, katika shughuli za uzalishaji mali, na ushiriki wake katika Miradi ya Kimkakati ikiwa ni pamoja na Ulinzi na Uangalizi wa Bonde la Mzakwe unaofanywa na Kikosi cha 834 Makutupora.
Ziara hiyo ilikuwa na lengo la Kufuatilia na kujionea hali ya mafunzo ya vijana na jinsi Jeshi la Kujenga Taifa linavyotekeleza majukumu yake ya msingi ya malezi ya vijana, uzalishaji mali na jukumu la Ulinzi wa Taifa.
Awali, akimkaribisha Waziri wa Ulinzi na JKT, Kamanda Kikosi 834 kikosi cha Jeshi, Luteni Kanali Petro Mbanga, alimfahamisha Waziri wa Ulinzi kuwa kikosi hicho kimeendelea kutekeleza majukumu yake ya mafunzo na malezi kwa vijana, uzalishaji mali na ulinzi wa Taifa kwa ufanisi, na akamfahamisha Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na JKT utayari wa kikosi hicho katika kushiriki shughuli zote na majukumu kitakachopangiwa na Serikali
Waziri Stergomena Tax katika ziara yake hiyo ya kikazi 834, alitembelea na kukagua sehemu za kulala vijana wa kike waliopo kikosini hapo kwa kujitolea na kwa mujibu wa Sheria.
Aidha, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alitembelea shughuli za Uzalishaji mali katika kiwanda cha vifungashio kilichopo kikosini hapo, kilimo cha mbogamboga katika green house, ufugaji wa kuku na mayai na nyama. Waziri wa Ulinzi na JKT alielezwa na Kamanda Kikosi jinsi vijana wanaofanya mafunzo wamekuwa wakinufaika kwa kupata mafunzo ya stadi za kazi kwa vitendo kupitia na miradi hiyo.