Huku dunia ikikabiliwa na uhaba wa chanjo za kipindupindu, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeidhinisha toleo jipya la chanjo hiyo kwa mdomo.
Inatarajiwa kwamba chanjo iliyo rahisi kutengeneza itasaidia kukabiliana na ongezeko la ugonjwa wa bakteria ambao kwa kawaida huenezwa kupitia chakula au maji yaliyochafuliwa.
Kupungua kwa hifadhi ya chanjo duniani kumeziacha nchi maskini zaidi, zikiwemo kadhaa barani Afrika, zikihangaika kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Ikiachwa bila kutibiwa, kipindupindu kinaweza kusababisha kifo ndani ya saa chache, hata kwa watu waliokuwa na afya njema hapo awali.
Toleo jipya, linaloitwa Euvichol-S, ni fomula iliyorahisishwa ambayo inatumia viungo vichache, ni ya bei nafuu, na inaweza kufanywa kwa haraka zaidi kuliko toleo la zamani.
Kuidhinishwa na WHO kunamaanisha mashirika ya wafadhili kama vile muungano wa chanjo Gavi na UNICEF sasa wanaweza kuinunua kwa nchi maskini zaidi, na kuongeza usambazaji.
Mkurugenzi wa kitengo cha ugavi cha UNICEF, Leila Pakkala, alisema kuwa shirika hilo litaweza kuongeza usambazaji kwa zaidi ya asilimia 25.
Gavi alikadiria kuwa kunaweza kuwa na dozi milioni 50 kwa hifadhi ya kimataifa mwaka huu, ikilinganishwa na milioni 38 mwaka jana.