Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma amesema Serikali inaendelea na mpango wa ukarabati wa viwanja mbalimbali vya michezo kwa awamu katika majiji, mikoa, Halmashauri na Manispaa zote nchini akieleza kuwa ukarabati wa uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ulipo Mkoani Tabora utakuwepo katika awamu zitakazofuata kwa kuwa Serikali imeanza na ukarabati wa viwanja vitano ambavyo ni Uhuru, Mkwakwani Tanga, Jamhuri Morogoro, Majimaji uliopo Songea na uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.
Mhe. Mwinjuma ametoa kauli hiyo leo April 19, 2024 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Hawa Mwaifunga aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa ukarabati mkubwa wa uwanja wa mpira wa Ali Hassan Mwinyi Tabora ili utumike kwenye mashindano ya AFCON 2027.
MHE. Mwinjuma ameongeza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa ukarabati wa uwanja wa Mpira wa Ali Hassan Mwinyi Tabora pamoja na viwanja vingine hapa nchini na imeendelea kuwasisitiza wadau na wamiliki wa viwanja kujenga na kutunza miundombinu hiyo sawa na maelekezo ya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995.
Aidha, amesema Serikali inajenga na kukarabati viwanja vitakavyotumika katika mashindano ya AFCON 2027 ambavyo ni Benjamin Mkapa, Aman Zanzibar na Uwanja mpya wa Dkt. Samia Suluhu Hassan unaojengwa katika Jiji la Arusha.