Madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekoutoure wamefanikiwa kufanya upasuaji na kuondoa Jiwe ndani ya kibofu cha Mkojo kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 48.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hospitalini hapo jiwe hilo lenye uzito wa Gramu 800 lilimsumbua mhusuka kwa zaidi ya miaka mitatu.
Akizungumza Aprili 18, 2024 na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekoutoure Dkt. Jackson Chiwaligo amesema hiyo ni mara ya kwanza kufanya upasuaji kama huo.
Dkt. Chiwaligo ameeleza kuwa mgonjwa huyo alifika Hospitali ya Sekoutoure akiwa na changamoto ya maumivu makali sehemu ya chini ya tumbo kwa zaidi ya miaka mitatu.
“Baada ya vipimo tuligundua kuwa na uvimbe mkubwa sehemu ya kibofu cha mkojo ulisababisha maumivu hivyo tukaona suluhisho iwe ni kufanyiwa upasuaji na kuondoa jiwe hilo lenye uzito wa Gramu 800”, amebainisha Dkt. Chiwaligo
Dkt. Chiwaligo ambaye aliwaongoza madakatari wenzake amesema uwepo wa jiwe kwenye kibofu ni mkusanyiko wa madini ya chumvi ambayo hukauka na kusababisha uvimbe kutokea katika kibofu cha mkojo.