Marehemu Mkuu wa Majeshi (CDF) Francis Ogolla, 62, anatazamiwa kuzikwa nyumbani kwake Ng’iya huko Alego Usonga mnamo Aprili 21 hii ni kwa mujibu wa familia yake.
Viongozi pia walifichua kwamba mazishi hayo yanakuja mapema kwa sababu Jenerali Ogolla alikuwa ameacha wosia na maagizo kwamba azikwe ndani ya saa 72 baada ya kifo chake.
Duru zilisema kuwa wanajeshi wamearifiwa kuhusu wosia huo na kufanya kazi ndani ya muda uliopangwa ili kuhakikisha kuwa unaheshimiwa.
Maandalizi ya mazishi yamechukuliwa na serikali. Hii ni kwa sababu alifariki akiwa ofisini.
Miili ya Jenerali Ogolla na maafisa wengine tisa wa kijeshi ilisafirishwa hadi Nairobi Alhamisi usiku.
Miili hiyo ilipokelewa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta katika kituo cha kijeshi cha Embakasi ambapo ibada ilifanyika.
Kisha ilisafirishwa kwa ambulensi hadi Hospitali ya Forces Memorial kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Siku ya Ijumaa, familia mbili za walioaga zilitembelea chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya utambuzi na uwezekano wa mazishi kulingana na taratibu za Kiislamu.
Chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana. Kikosi cha wataalam kilikwenda hadi eneo la tukio mnamo Ijumaa kuanza uchunguzi, maafisa walisema.
Ogolla aliaga pamoja na maafisa wengine wanane wa kijeshi Alhamisi alasiri katika ajali ya helikopta huko Marakwet Mashariki walipokuwa kwenye oparesheni ya amani katika maeneo mbalimbali ya eneo la North Rift.
Wengine wawili, hata hivyo, walinusurika katika tukio hilo la kusikitisha. Mabaki ya hao tisa yanahifadhiwa Nairobi.