Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema Serikali imefanya maboresho viwango vya posho za kujikimu Wasimamizi wa Uchaguzi kwa kuzingatia Waraka wa Utumishi wa Umma kuhusiana na posho za serikali.
Amesema hayo hii leo Aprili 22, 2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Angelina Malembeka, ambaye amehoji Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu Mpango wa kuongeza posho kwa Askari na Maafisa Wasimamizi wa Uchaguzi.
Akijibu swali hilo, Mhe. Katambi amesema kuwa wakati wa uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata hulipwa posho za kujikimu wanapokuwa wakitekeleza majukumu ya uchaguzi.
Ameongeza kuwa, Watendaji na Walinzi wa vituo vya kupigia kura utaratibu wa uboreshaji wa viwango vyao vya posho utazingatiwa wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Bajeti ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.