Idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza imeongezeka hadi 34,097, Wizara ya Afya inayoongozwa na Hamas ilisema katika taarifa yake Jumapili.
Jeshi la Israel liliwauwa Wapalestina 48 na kuwajeruhi wengine 79 katika muda wa saa 24 zilizopita, na kufanya jumla ya waliofariki kufikia 34,097 na majeruhi kufikia 76,980, tangu kuzuka kwa mzozo kati ya Israel na Hamas Oktoba 7, 2023.
Mahmoud Basal, msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi katika Ukanda wa Gaza, aliwaambia waandishi wa habari kwamba waokoaji wameopoa miili zaidi ya 50 kutoka maeneo mbalimbali katika mji wa Khan Younis. Jeshi la Israel lilijiondoa kutoka kwa Khan Younis mnamo Aprili 7, miezi minne baada ya kuanzisha operesheni ya ardhini.
Basal amesema miili hiyo imezikwa kwa pamoja na jeshi la Israel na kuongeza kuwa operesheni za kuwasaka zinaendelea kwani maelfu ya watu bado hawajapatikana huko Gaza.
Msemaji huyo alishutumu jeshi la Israel kwa “kutekeleza upotevu wa watu katika Ukanda wa Gaza kwa utaratibu na kwa makusudi.”
Majeshi ya Israel “yaliharibu makumi ya miili” kabla ya kuwazika na kuondoka, alisema.
Israel ilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza kulipiza kisasi dhidi ya uvamizi wa Hamas kupitia mpaka wa kusini wa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na zaidi ya 200 walichukuliwa mateka.