Mtoto mmoja ameripotiwa kufariki dunia na karibu watu 2,500 wamepoteza makazi yao baada ya maporomo ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa kuharibu takriban nyumba 500 na kuharibu kabisa bwawa la kuzalisha umeme huko Gitaza, wilaya ya Muhuta, mkoa wa Rumonge, kusini magharibi mwa Burundi.
Gavana wa Mkoa wa Rumonge, Abdul Ntiranyibagira amethibitisha habari hiyo na kufafanua kwa kusema: “Kijiji kilichoathirika zaidi ni Gabaniro. Mtoto wa miaka minne amefariki dunia kwenye kijiji hicho na hakuna nyumba iliyobaki imesimama wima kijijini hapo. Jumla ya nyumba 497 zimeharibiwa na kuwaacha watu 2,485 bila makazi kutokana na maporomoko hayo.”
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa wa Rumonge, zaidi ya hekta 500 za mashamba ya mazao zimeharibiwa katika maporomoko ya ardhi yaliyotokea kwenye kijiji cha Gabaniro na vijiji jirani.
Amefafanua zaidi kwa kusema: “Udongo uliporomoka kutoka kwenye mlima na kushuka chini ya mto Kirasa, na kuharibu kabisa bwawa la kufua umeme lililokuwa linazalisha umeme wa mji wa Mutumba katika wilaya hiyo hiyo ya Muhuta. Maporomoko hayo pia yameharibu kabisa majengo yote ya karibu na bwawa hilo.”
Amedokeza kuwa, watu waliopoteza makao yao wamesitiriwa katika Skuli ya Ufundi ya Gitaza.
Pia amesema: “Kwa sababu za kiusalama, tumewaambia watu wote waliokuwa wakiishi katika kijiji cha Gabaniro na wengineo wa karibu na vijiji vilivyoathiriwa na maporomoko ya udongo, kuondoka eneo hilo na kukaa kwa muda katika Skuli ya Ufundi ya Gitaza hadi hapo hatua nyingine zitakapochukuliwa.”