Mkuu wa kitengo cha kijasusi cha jeshi la Israel amejiuzulu kutokana na kushindwa kwa kitengo chake wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas.
“Iliamuliwa kuwa MG Aharon Haliva atamaliza wadhifa wake na kustaafu kutoka kwa IDF, mara tu mrithi wake atakapoteuliwa kwa utaratibu mzuri na wa kitaalamu,” Jeshi la Ulinzi la Israel lilisema katika taarifa siku ya Jumatatu.
Meja Jenerali Aharon Haliva, ambaye amehudumu katika IDF kwa miaka 38, ndiye mwanajeshi wa kwanza mkuu kujiuzulu kutokana na mashambulizi ya Oktoba 7, wakati wapiganaji wa Hamas walipovamia mpaka na Israel.
Shambulio hilo lilionekana kufeli kwa kiwango kikubwa cha kijasusi cha Israel, huku maafisa kadhaa wakuu wa ulinzi na usalama wakijitokeza mwezi Oktoba kuwajibika kwa kiasi fulani kwa makosa yaliyosababisha mashambulizi hayo.
Kufuatia shambulio lililoikumba Israel, Haliva alikiri kushindwa kwa kijasusi na kitengo chake kutogundua mipango ya Hamas.
“Hatukutimiza kazi yetu muhimu zaidi, na kama mkuu wa Kurugenzi ya Ujasusi, ninachukua jukumu kamili kwa kushindwa huku,” alisema wakati huo.