Mkurugenzi wa gereza la Ecuador linalojulikana kama “El Rodeo” aliuawa Jumapili katika shambulizi lililotokea wakati mamilioni ya watu nchini humo wakielekea kwenye kura ya maoni iliyolenga zaidi vita vya Rais Daniel Noboa dhidi ya uhalifu.
Afisa huyo alitambuliwa katika taarifa ya shirika la magereza la Ecuador, SNAI kama Cosme Damián Parrales Merchán, mkurugenzi wa gereza la eneo la Manabi, lakini hakuna maelezo zaidi kuhusu kifo chake yalishirikiwa.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Ecuador iliripoti kuwa mtu mwingine alijeruhiwa katika shambulio hilo na kwamba maafisa waliokuwa kwenye eneo la tukio wameanza uchunguzi. Hakuna aliyekamatwa hadi sasa.
SNAI ilisema itafanya kazi na mamlaka za mitaa kuchunguza mauaji ya Parrales na kusema kwamba kifo chake kinaleta “huzuni kwa Mfumo mzima wa Kitaifa wa Urekebishaji wa Jamii.”