Mkoa wa Shingaya waanza rasmi utoaji chanjo ya saratani ya mlango wa shingo ya kizazi (HPV), kwa watoto wa kike, huku serikali ikionya kuwa yeyote atakayebainika kupotosha kuhusu chanjo hiyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Akizungumza katika uzinduzi huo ambao umefanyika leo Aprili 22, 2024 katika Shule ya Msingi Ndala “A” iliyopo Manispaa ya Shinyanga, mkuu wa mkoa huo, Anamringi Macha, amesema kumekuwa na desturi ya watu kupotosha juu ya chanjo mbalimbali.
“Chanjo hii ya saratani ya mlango wa shingo ya kizazi ni salama kabisa na haina madhara yoyote, na ilianza kutolewa tangu mwaka 2014, na tangu kipindi hicho hakuna madhara yoyote ambayo yametokea, sasa kwa wale ambao wataanza upotoshaji Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria,” amesema na kuongeza;
“Mwananchi yoyote ambaye hana uelewa kuhusu chanjo hii, ni vyema akafika kwenye vituo vya huduma za afya au maeneo ambayo chanjo inatolewa (mashuleni), aulize na kuelimishwa kuliko kuanza kuandika kwenye mitandao ya kijamii na kufanya upotoshaji au kwenye vijiwe, tukikubaini tutakuchukulia hatua.”
Aidha mkuu wa mkoa huyo amesema Serikali haiwezi kuleta chanjo yenye madhara kwa wananchi wake, na kwamba HPV imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), na kuwataka wazazi wasiwe na wasiwasi dhidi ya chanjo hiyo.
Mkoa wa Shinyanga umejiwekea lengo la kuwafikia watoto wa kike 198, 865; wenye umri wa kuanzia miaka 9 – 14; lengo likiwa ni kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi.
Hivyo ametoa wito kwa wazazi kuwaruhusu watoto wao wachanjwe ili kuwakinga na ugonjw ahuo, huku akiwataka walimu pamoja na wataalamu wa afya, kuhakikisha utoaji chanjo hiyo, auharibu vipindi vya masomo.