Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala kuwasilisha majina ya Mameneja wa Kanda na Mikoa wa TEMESA ambao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi ili waweze kuchukuliwa hatua.
Bashungwa ametoa agizo hilo Aprili 22, 2024 jijini Dodoma kufuatia kupokea malalamiko mara kwa mara kuhusu huduma zinazotolewa na TEMESA ikwemo huduma ya Kivuko cha MV.Tanga Mkoani Tanga ambapo amemuagiza Katibu Mkuu kuingilia kati kubaini changamoto zinazokwamisha kivuko hicho.
“Mambo mengi ya kiutendaji yanaletwa kwa Waziri na Katibu Mkuu wakati Watendaji mpo na tumewaamini kusimamia Taasisi zenu, hasa jambo hili lipo TEMESA. Mtendaji Mkuu kama kuna mapungufu ya wasaidizi wako bora uje kwa Katibu Mkuu useme huyu atufahi aondoke kuliko kukaa nao maana hatimaye litakuangukia wewe”, amesema Bashungwa.
Bashungwa amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour kuangalia namna bora ya usimamizi wa TEMESA katika huduma ya vivuko nchini ili kuleta manufaa na uboreshaji wa huduma za usafiri na usafirishaji ziimarike.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa bado TEMESA inaendelea kuwa na mikwamo na kutotekeleza majukumu yake kwa uharaka pindi tatizo linapogundulika katika Vivuko na hivyo kupelekea kuzorota kwa huduma hiyo katika baadhi ya maeneo.
“Changamoto ya marekebisho ya kivuko cha MV Tanga yanaendelea zaidi ya siku 10 sasa lakini leo naulizia vifaa bado havijafika, kama ‘parts’ ziko Dar es Salaam inachukua masaa mangapi hadi kufika Tanga? na sio Tanga pekee yake ni maeneo yenye vivuko”, Bashungwa akimuhoji Mtendaji Mkuu wa TEMESA.