Takriban watu 2,500 wameuawa, kujeruhiwa au kutekwa nyara nchini Haiti kutokana na ghasia za magenge kufikia sasa mwaka huu, mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) alisema Jumatatu.
Akizungumza katika mkutano na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Haiti, Catherine Russell alielezea hali ya nchi hiyo kuwa ya “janga,” akionya kuwa inazidi kuwa mbaya zaidi siku hadi siku.
“Watu milioni tano na nusu, wakiwemo watoto milioni tatu – au wawili katika kila watoto watatu nchini kote – wanahitaji msaada wa kibinadamu,” alisema.
Russell alikariri kwamba miaka mingi ya msukosuko wa kisiasa na hali mbaya ya kiuchumi imesababisha kuenea kwa makundi yenye silaha.