Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergey Shoigu amesema, hasara za kijeshi ilizopata Ukraine za kuuawa askari wake tangu Februari 2022 hadi sasa zimefikia karibu wanajeshi 500,000.
Akihutubia mkutano wa mawaziri, Shoigu amefafanua kuwa, vikosi vya Russia vina mkakati vinaotekeleza kwenye mstari wa mbele wa mapigano na vinawarudisha nyuma wapinzani wao; na akaongeza kuwa, shinikizo hilo la vikosi hivyo linawazuia wanajeshi wa Kiev na kuwafanya wabaki kwenye hali ya kujihami.
Waziri wa Ulinzi wa Russia amezungumzia pia msaada wa kijeshi wa zaidi ya dola bilioni 60 unaotarajiwa kutolewa na Marekani kwa Kiev na akabainisha kuwa, hatua hiyo inalenga “kuzuia kusamabaratika” kwa vikosi vya Ukraine, lakini akatabiri kwamba, fedha hizo hazitaathiri kwa kiasi kikubwa hali katika medani ya vita, kwa kuwa nyingi zake zitaenda kwenye sekta ya uundaji silaha ya Marekani.