Kupitia maadhimisho ya miaka 25 ya huduma ya Compassion Tanzania,wadau wanaoshirikiana nao ambao ni vituo vya huduma ya maendeleo ya mtoto na kijana klasta ya Bukoba wameiomba serikali kupitia ustawi wa jamii kuwasaidia kutatua changamoto ya baadhi ya vituo vya kutolea huduma ya afya kukataa Bima ya Afya wanayotumia kuhudumia watoto wanaowalea.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa wachungaji klasta ya Bukoba Askofu Godfrey Batholomeo ambao mpaka sasa wamewafikia watoto na vijana zaidi ya 1450 lengo likiwa ni kutoa huduma kwao katika maeneo ya kiroho,kiakili,kijamii na kimwili.
Aidha katika wiki ya maadhimisho ya miaka hiyo 25,klasta ya Bukoba wamefanikiwa kutembelea na kutoa faraja kwenye vituo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Bukoba huku wakiahidi kuendelea kusaidia jamii ya wahitaji kwa maana ya kumkomboa mtoto kutoka kwenye umasikini kwa jina la Yesu,kwani hufanya hivo mara nyingi ikiwemo kuboresha makazi ya wahitaji sambamba na kusaidia huduma za matibabu.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Rebeka Gwambasa ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera amewaondolea hofu upande wa changamoto ya bima ya afya wanayoitumia na kuwaomba watakapozuiliwa watoe taarifa katika ofisi yao ili waweze kufanyia kazi changamoto hiyo kwa kituo husika sambamba na kuahidi kuendelea kuonyesha ushirikiano kwao ili kuhakikisha wanakomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto huku akiwataka kuweka wazi na kutoa ushirikiano kwenye vyombo vya ulinzi na usalama pindi wanapobaini uwepo wa vitendo hivyo na mwisho wa siku waweze kuiishi kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayoeleza, malezi bora kwa ulinzi wa mtoto.