TAASISI ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha huduma mpya ‘Home Based Care’ kwa wagonjwa wa moyo wa nyumbani ambao watawekewa shuka maalum lenye kifaa kitakachotoa taarifa moja kwa moja hospitalini za mapigo ya moyo, umeme wa moyo na hali ya presha kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, akifafanua kuwa, shuka hilo maalum litakuwa na kifaa kitakachowezesha wataalam walioko JKCI kupata taarifa za mgonjwa aliyeko nyumbani moja kwa moja.
Dk. Kisenge ambaye ni Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, amesema mgonjwa akihitaji huduma ya saa 24 akiwa nyumbani atapewa kupitia daktari au nesi.
Amesema kupitia huduma hiyo watawahudumia wagonjwa wakiwa nyumbani hususani waliokuwa wamelazwa JKCI na kuruhusiwa, lakini bado wanahitaji uangalizi maalum.
“Wakiwa nyumbani tutaendelea kuwahudumia. Tumekuja na huduma mpya kabisa ya teknolojia ya juu ambapo mgonjwa atalalia shuka maalum na kuweka kifaa maalum chini ya kitanda chake na sisi tutaweza kugundua mapigo ya moyo au umeme wa moyo na tutagundua presha zake zikoje.
“Tutaweza kujua oksijeni yake ikoje kwa kuwa wagonjwa waliozidiwa sana presha hushuka ghafla na kupoteza maisha. Akiwa nyumbani tutapata ujumbe kwamba mgonjwa yupo nyumbani na presha zimeshuka na itakuwa rahisi kumfuata aliko,” amesema.
Dk. Kisenge amesema JKCI ina magari ya wagonjwa zaidi ya sita, wanaweza kumfuata mgonjwa na kumpeleka hospitalini hapo na kumhudumia.
Kupitia teknolojia hiyo mpya ambayo inatumika nchini India, wanaweza kumwambia ndugu nini cha kufanya.