Serikali itaendelea kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kutoka hekta 727,280 msimu wa 2022/2023 hadi kufikia hekta 1,200,000 ifikapo 2025, kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora za mazao zinazohimili mabadiliko ya tabianchi na usambazaji wa mbolea kwa mpango wa ruzuku ili kuweza kukabiliana na tatizo la njaa nchini.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amesema hayo tarehe 23 Aprili 2024, Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mhe. Jackson Kiswaga, Mbunge wa Kalenga kuhusu Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la njaa nchini linalotokana na upungufu wa mvua.
”Nchi yetu imekuwa ikijitosheleza kwa chakula kwa kigezo cha upimaji wa utoshelevu (Self Sufficiency Ratio – SSR), kati ya asilimia 112 hadi 126 kwa kipindi cha miaka kumi (10) mfululizo. Aidha, kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kusababisha upungufu wa mvua na kuhatarisha usalama wa chakula, Serikali inaendelea kuchukua hatua,” ameeleza Mhe. Silinde.
Amesema katika mwaka ujao wa Fedha 2024/2025 Serikali itajenga mabwawa mapya mia moja (100) ya umwagiliaji ikiwemo katika jimbo la Kalenga ili kuweza kusaidia changamoto za mvua nyingi ambazo zimekuwa zikileta Madhara na kusaidia pale kunapokuwa na uhaba wa mvua.
Serikali pia itaendelea kuimarisha miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya chakula kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutoka tani 360,000 hadi tani 500,000 ifikapo 2025. Hadi kufikia Aprili, 2024 NFRA imenunua na kuhifadhi tani 294,069.216 kwa ajili ya kusambazwa katika maeneo ambayo yatabainika kuwa na upungufu wa chakula.