Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko (Mb), leo Aprili 24, 2024 amewasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 katika Mkutano wa Kumi na Tano Kikao cha Kumi na Tatu.
Miradi ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme
1.Miundombinu imara ya kusafirisha na kusambaza umeme ndiyo msingi thabiti wa kuwa na umeme wa uhakika. Hatua zitakazochukuliwa na Serikali katika mwaka 2024/25 ni pamoja na kukamilisha mradi wa kusafirisha umeme kutoka Julius Nyerere Hydro Power Plant hadi Chalinze – Kilovoti 400 na Kituo cha Kupoza Umeme, Chalinze ambapo kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kumalizia kazi zilizobaki katika kituo cha kupoza umeme ikiwemo majengo, barabara, njia ya kusafirisha umeme na marekebisho mbalimbali.
2.Serikali itaendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345 na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme vya Chalinze na Dodoma.
3.Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha kusafirisha umeme unaotoka katika Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere kupitia Chalinze, kwenda mkoani Dodoma na kuusambaza katika mikoa mbalimbali nchini.
4.Miradi mingine ya usafirishaji wa umeme itakayotekelezwa ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze – Kinyerezi – Mkuranga; ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme Msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze – Segera na msongo wa Kilovoti 220 Segera – Tanga;
5.Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 220 kutoka Chalinze – Bagamoyo hadi Ununio Dar es salaam na ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ibadakuli Shinyanga Kilovoti 400/220/33; ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma (TAZA) na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma.
6.Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization Project) – Gridi Imara kwa kuendelea na ujenzi wa njia za kusafirisha umeme pamoja na vituo vya kupoza umeme.
7.Serikali pia itaendelea kufanya matengenezo katika mitambo ya kuzalisha umeme, miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme pamoja na vituo vya kupoza umeme ili kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana wakati wote.