BAADHI ya wanafunzi na walimu wa shule za sekondari mkoani Geita wamesema zoezi la ugawaji wa taulo za kike kwa ajili ya kuwasitiri wanafunzi wa kike kipindi cha hedhi, limechangia kupunguza utoro wa wanafunzi hao katika masomo mbalimbali wanapokuwa kwenye siku za hedhi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti hivi karibuni, wanafunzi na walimu hao wameishukuru Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kutatua changamoto hiyo ya usimamizi wa usafi wa hedhi katika shule mbalimbali za mkoa huo.
Wamesema tangu GGML ianze ugawaji wa taulo hizo za kike na kufanya zoezo hilo kuwa endelevu, limebadiliha matokeo ya ufaulu na hata maisha ya maisha yao.
Mmoja wa wanafunzi hao, Kulwa Lameck ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Nyakabale, amesema zoezi hilo limewasaidia kujitambua kutokana na elimu ya afya ya hedhi wanayopatiwa.
“Elimu ya usafi wa hedhi tuliyoipata kutoka GGML ni muhimu sana kwa sababu imenipa ujasiri zaidi, najiona niko huru muda wote, hata wakati wa hedhi, sihitaji kuhangaika sasa najua cha kufanya na kuwa na vifaa vya kunisaidia. Na kujiweka vizuri,” alisema Kulwa.
Naye Mwalimu wa Shule ya Sekondari Nyankumbu, Rosemary Nicolaus, alisema ameona mabadiliko makubwa katika mahudhurio ya wanafunzi wake na ufaulu wao wa kielimu tangu walipopata mafunzo ya usafi wakati wa hedhi.
“Baada ya elimu ya usafi wakati wa hedhi, mahudhurio ya watoto wa kike yameongezeka kwa kiasi kikubwa, na imani yao katika masomo imeongezeka. Hii imekuwa mabadiliko chanya kwa wasichana wetu, imeangaza maisha yao ya sasa na ya baadaye,” anasema.
Aidha, alisema changamoto zinazowakabili wasichana wa mkoa wa Geita pia zinawakabili wengine katika mikoa mbalimbali nchini, hivyo ni vema wadau mbalimbali waendelee kuungana mkono dhana ya kutoa misada ya taulo za kike na elimu ya afya ya uzazi kwa wanafunzi wa kike ili waweze kujisitiri na kuondokana na dhana potofu.
Kwa upande wake Emily Zachariah, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Nyakabale naye alisema; “Sasa najua kuwa hedhi ni sehemu muhimu ya uumbaji kwa wasichana, ni jambo la kawaida na ni sehemu ya maisha yao, linahitaji kuthaminiwa na kuheshimiwa.
“Mabadiliko haya ya kimtazamo, yakisaidiwa na mipango ya GGML, ni hatua ya kwanza kuelekea siku za usoni ambapo hedhi si chanzo cha aibu tena, bali ni sehemu ya uzoefu wa maisha ya mwanadamu,” alisema.
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), zinaonesha kuwa kila siku wanawake na wasichana milioni 300 hawana mazingira mazuri ya kujisitiri pindi wanapokuwa kwenye kipindi cha hedhi, hawana yaulo za kike wala elimu ya afya ya uzazi kuhusu usafi wa hedhi.
Shirika hilo linaeleza kuwa kutokana na hali hiyo wanfunzi wa kike hushindwa kuhudhuria darasani kwa siku 40 katika mwaka kutokana na changamoto za hedhi.