Vikosi vya kijeshi nchini Burkina Faso viliwauwa raia 223, wakiwemo watoto wachanga na watoto wengi, katika mashambulizi dhidi ya vijiji viwili vinavyodaiwa kushirikiana na wanamgambo, Human Rights Watch ilisema katika ripoti iliyochapishwa Alhamisi.
Mauaji hayo ya umati yalifanyika Februari 25 katika vijiji vya kaskazini mwa nchi hiyo vya Nondin na Soro, na watoto wapatao 56 walikuwa miongoni mwa waliofariki, kulingana na ripoti hiyo. Shirika hilo la kutetea haki za binadamu lilitoa wito kwa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kutoa wachunguzi na kuunga mkono juhudi za ndani kuwafikisha waliohusika mbele ya sheria.
“Mauaji katika vijiji vya Nondin na Soro ni mauaji ya hivi punde zaidi ya raia yaliyofanywa na jeshi la Burkina Faso katika operesheni zao za kukabiliana na waasi,” Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch Tirana Hassan alisema katika taarifa yake. “Msaada wa kimataifa ni muhimu kusaidia uchunguzi wa kuaminika kuhusu uhalifu dhidi ya ubinadamu.”
Taifa hilo lililokuwa na amani limekumbwa na ghasia ambazo zimewakutanisha wanajihadi wanaohusishwa na al-Qaida na kundi la Islamic State dhidi ya vikosi vinavyoungwa mkono na serikali. Pande zote mbili zimelenga raia waliopatikana katikati, na kuwafukuza zaidi ya watu milioni 2, ambao zaidi ya nusu yao ni watoto. Mashambulizi mengi hayaadhibiwi na hayaripotiwi katika taifa linaloendeshwa na uongozi dhalimu unaowanyamazisha wanaodhaniwa kuwa ni wapinzani.