Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila itaendelea kujikita katika kuanzisha huduma mpya za ubingwa bobezi hapa nchini ili kuwapunguzia wananchi gharama na usumbufu wa kutafuta huduma hizo nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Godlove Mfuko alipokuwa akiongea katika kongamano la kitaalam liliondaliwa kwa ushirikiano wa MNH-Mlogazila na Hospitali za HCG za nchini India kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalam kuhusu upasuaji wa upandikizaji wa ini.
Dkt. Mfuko ameongeza kuwa kutokana uwekezaji uliofanywa na Serikali nchini ambao umeleta mapinduzi makubwa katika kutoa huduma za afya, hivyo ni wajibu wa Mloganzila kutoa huduma ambazo hazipatikani nchini na kuimarisha huduma zilizopo kwa kuendelea kuwajengea uwezo wataalam.
“Baada ya uwekezaji uliofanywa na Serikali, sisi kama wataalam kazi yetu ni kujituma na kufikiri kwa namna gani Hospitali ya Taifa inachangia kuanzisha huduma za ubingwa bobezi ikiwemo kupandikiza ini hapa nchini na inawezekana” ameongeza Dkt. Mfuko
Kwa upande wake Daktari Bingwa Bobezi wa upasuaji ambaye pia amebobea katika masuala ya upandikizaji wa ini kutoka Hospitali za HGC, Dkt. Basant Mahadevappa amesema huduma ya upasuaji wa upandikizaji wa ini unahitaji maandalizi muhimu ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa kada mbalimbali.