Takriban wafungwa 118 wametoroka gerezani baada ya mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia leo ikipelekea uharibifu wa gereza la Suleja karibu na mji mkuu wa Abuja nchini Nigeria, msemaji wa magereza hilo alisema.
Mvua zilizonyesha kwa saa kadhaa, ziliharibu sehemu kubwa za gereza ikiwa ni pamoja na ukuta na majengo yanayozunguka, msemaji wa gereza hilo Adamu Duza alisema katika taarifa mapema hii leo huku maafisa wa magereza wakianza operesheni ya kuwawinda wafungwa hao waliotoroka huku mpaka sasa wamewakamata 10 kwa usaidizi wa mashirika mengine ya usalama.
Msemaji wa gereza la Suleja alisema wapo mbioni kuwakamata wafungwa wote waliosalia akiihakikishia umma kuwa mamlaka inafanya juhudi zote kufanikisha jambo hilo.
Duza hakutoa maelezo zaidi juu ya majina au uhusiano wa wafungwa waliotoroka lakini hapo awali wanachama wa kundi la waasi la ‘Boko Haram’ waliripotiwa kufungwa katika gereza hilo.
Maelfu ya wafungwa wameripotiwa kutoroka katika miaka ya hivi karibuni kutokana na miundombinu hafifu, msongamano wa wafungwa pamoja na mashambulizi ya wanamgambo, hasa shambulio la Julai 2022 la kundi la ‘Islamic State’ kwenye gereza lenye ulinzi mkali katika mji mkuu wa Abuja ambapo takriban wafungwa 440 walitoroka.