Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha shilingi Trilioni 1.8 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati katika mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo asilimia 95 ya bajeti hiyo imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akijibu hoja mbalimbali za Wabunge ameeleza kuwa, ili wananchi wanaozunguka miradi ya Gesi Asilia na Mafuta wafaidike na rasilimali hiyo Serikali itapitisha kanuni itakayoongoza Miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) ili kampuni ziweze kuwajibika ipasavyo kwa jamii.
Aidha, kuhusu ushuru wa huduma (service levy) unaotolewa na kampuni za Mafuta na Gesi kwa Halmashauri mbalimbali nchini, Dkt. Biteko ameagiza Halmashauri hizo zihakikishe kuwa sehemu ya fedha hizo zinarudi kwenye vijiji ambapo miradi inatekelezwa.
“Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wasiliana na Katibu Mkuu TAMISEMI ili kuja na mpango wa utekelezaji wa service levy ili fedha zinazotolewa ziende pia kwenye maeneo ambapo miradi inatekelezwa, Rais ameshaeleza hataki kuona malalamiko sehemu ambapo Gesi inachimbwa, Service Levy na CSR sasa zitaanza kufanyiwa kazi kwa kasi kubwa.” Amesema Dkt. Biteko
Amesisitiza kuwa, suala la CSR si siri bali ni kitu cha wazi kwa wananchi na Wabunge hivyo ni haki kwa wananchi hao kupata taarifa za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii na kusisitiza kampuni za kitanzania kupewa kipaumbele kwenye miradi ili wananchi wanufaike na rasilimali zilizopo nchini.
Kuhusu hali ya kukatika kwa umeme mara kwa mara miezi kadhaa nyuma, amesema ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na upungufu wa umeme wa megawati 410 lakini sasa uwezo wa kuzalisha umeme umekuwa mkubwa kuliko mahitaji huku mitambo minne ya Kinyerezi ikizimwa na kusubiri changamoto itakayojitokeza.