Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuendelea kuwapa maua yao na kudumisha maono ya Waasisi wa Muungano Hayati Mwl. Nyerere na Mzee Karume pamoja na Viongozi waliofuatia baada yao, kutokana na juhudi zao za kuujenga na kuudumisha Muungano.
Rais Samia amesema hayo leo April 26,2024 wakati akitoa hotuba yake katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam wakati wa Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Nawatakia Watanzania wote kheri ya kutimiza miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, kwa niaba yenu Watanzania nawashukuru kwa dhati Waasisi wa Muungano Mwl.Nyerere na Mzee Karume pamoja na Viongozi waliofuata baada yao kwa kutuleta pamoja na kujenga Taifa huru, madhubuti na lenye matumaini , zawadi pekee tunayoweza kuwapa ni kuendelea kudumisha Muungano huu na kuyaenzi maono yao kwa msemo wa siku hizi tunasema tuwape maua yao”
“Waswahili tunaamini shughuli na kama mnavyoona pamoja na baraka ya mvua lakini Watu wamejitokeza kwa wingi kwenye shughuli hii, tumepata heshima ya kuungwa mkono na Wakuu wa Nchi nq Serikali kutoka SADC na Jumuiya ya Afrik Mashariki na wapo Viongozi waliokuja kuwawakilisha Marais wa Nchi zao”