Serikali ya Rwanda imesema madai ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waliyoyatoa wiki iliyopita kuishutumu Kampuni ya Apple kununua madini yanayosafirishwa kinyume na sheria kutoka Congo kupitia Rwanda, ni maoni yasiyo na msingi na ya kupuuzwa.
Kauli hii ya Rwanda imetolewa baada ya Congo kuishtumu Kampuni hiyo kutumia kwenye bidhaa zake madini hayo yanayosafirishwa kinyume cha sheria kutoka nchini humo na kuingizwa Rwanda.
Jana Ijumaa, Msemaji wa Serikali ya Rwanda Yolande Makolo aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba hii ni hatua ya hivi karibuni zaidi ya Serikali ya Kongo ambayo inajaribu kwa mara nyingine kuipaka matope Rwanda kwa shtuma za uongo.
Siku ya Alhamisi, Mawakili wa Congo waliishtumu Kampuni ya Apple kwa kununua madini yaliochimbwa kutoka mashariki mwa Nchi hiyo na kuingizwa Rwanda kinyume cha sheria na kisha baadae kusafirishwa na kuingizwa katika Soko la kimataifa.
Mawakili hao wa Congo pia waliwasilisha notisi rasmi kwa Apple kuionya kwamba huenda ikakabiliwa na hatua za kisheria ikiwa itaendelea kununua madini hayo, @dw_kiswahili wameripoti.