Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (UNOCHA) imesema, migogoro na maafa ya asili imewalazimisha zaidi ya watoto milioni 4.1, sawa na asilimia 35 ya idadi ya jumla ya wanafunzi kwa mwaka huu katika mkoa wa Amhara nchini Ethiopia, kukatiza masomo yao.
Kwa mujibu wa takwimu za UNOCHA, hali ya wasiwasi inayoendelea na athari za mgogoro uliodumu kwa miaka miwili kaskazini mwa nchi hiyo, imezifanya shule 4,178 katika eneo hilo kufungwa.
Ofisi hiyo pia imesema, takriban shule 300 katika sehemu mbalimbali mkoani humo zimeharibiwa, na shule 350 zimefungwa kutokana na migogoro na ukosefu wa usalama, na kwamba baadhi ya wilaya mkoani humo zimefunga shule kutokana na ukosefu wa vifaa vya shule.
Imeongeza kuwa watoto milioni 1.7 katika eneo hilo wanahitaji vifaa vya masomo, wakati zaidi ya walimu na wafanyakazi 56,000 wa elimu wanahitaji msaada wa kisaikolojia na kijamii.