Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema, karibu watu 88,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani nchini Somalia katika miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu.
Shirika hilo limesema, watu hao wamekosa makazi kutokana na mapigano ama ukosefu wa usalama na athari za muda mrefu za mafuriko, ambayo yametokea kati ya mwezi Oktoba na Desemba mwaka jana.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni iliyotolewa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, UNHCR imesema mapigano ya kikabila na tofauti za kisiasa ndani ya mikoa inayojiendesha na kati ya serikali ya Somalia na mikoa hiyo imetishia zaidi hali tete ya usalama nchini humo.
Shirika hilo limesema mapigano yaliyodumu kwa miongo mingi, mvutano wa kisiasa, mienendo ya kikabila na mabadiliko ya tabianchi vimesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu.